13: Dayalisisi

Dayalisisi

Wakati figo hazifanyi kazi yoyote,dayalisisi ni njia ya bandia ya kutoa uchafu na maji yasiyohitajika mwilini.Njia bora ya kuokoa maisha kwa watu ambao figo zao zimedhoofika kabisa.

Dayalisisi huwasaidiaje wagonjwa wenye figo zisizofanya kazi?

Dayalisisi husaidia mwili kwa kufanya kazi ambazo omit zingalifanywa na figo ambazo sasa hazifanyi kazi kama ifuatazo:

  • Kusafisha damu kwa kutoa uchafu kama kreatinini na yurea mwilini.
  • Kutoa maji yasiyohitajika mwilini na kusawazisha kiwango kinachofaa mwilini.
  • Kurekebisha usawa wa kemikali kama chumvi,potasiamu na magadi mwilini.

Hata hivyo,dayalisisi haiwezi kufanya kazi za figo za kawaida kama vile kudumisha himoglobini kwa kutengeneza eraithropoyetini wala kudumisha mifupa yenye afya.

Dayalisisi huhitajika lini?

Kazi ya figo inapopungua kwa asilimia themanini na tano au tisini(kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo - ESKD),figo basi huwa hazitoi uchafu na maji ya kutosha kutoka mwilini.Hali hii husababisha dalili kama kichefuchefu,kutapika,kuchoka,kuvimba na kushindwa kupumua.

Katika kipindi hiki cha ugonjwa sugu wa figo,dawa huwa hazifanyi kazi na basi dayalisisi huhitajika.Mgonjwa huhitaji dayalisisi, vipimo vya damu vinapoonyesha kreatinini ya 8.0mg/dl au zaidi kwenye damu.

Dayalisisi ni njia ya haraka na bora ya kutibu wagonjwa wenye figo zilizodhoofika zaidi.

Je,dayalisisi inaweza kuponesha ugonjwa sugu wa figo?

La hasha!Ugonjwa sugu wa figo hauponi kwa hiyo mgonjwa aliye katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa huu huhitaji dayalisisi maisha yake yote,isipokuwa akipatiwa figo nyingine.

Kwa upande mwingine,mtu mwenye ugonjwa wa figo wa muda huhitaji dayalisisi kwa muda mfupi tu hadi figo zitakapopona / zitakaporudia kazi yake kama kawaida.

Aina za dayalisisi

Kuna aina mbili kuu ya dayalisisi

  1. Dayalisisi ya damu.
  2. Dayalisisi ya tumbo.

Dayalisisi ya damu

Hii ndiyo njia inayotumika sana kutibu wagonjwa walio katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo.Hufanywa kwa kutumia figo bandia na mashine ya dayalisisi kutoa uchafu na maji yasiyohitajika kwenye damu.

Dayalisisi ya tumbo

Dayalisisi ya tumbo pia ni njia bora ya kutibu kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo – (ESKD). Hapa,mpira laini unaoitwa katheta huingizwa katika tumbo.Kupitia katika kimpira hiki au tyubu hii,maji ya dayalisisi huingizwa kwenye tumbo na hutoa uchafu na maji yasiyohitajika mwilini.Njia hii huweza hutumiwa nyumbani bila ya mashine.

Dayalisisi haiponyi figo lakini humsaidia mgonjwa kuendelea kuishi vyema ingawaje figo hazifanyi kazi.

Ni mambo gani yanayozingatiwa ili kuamua aina ya dayalisisi itakayotumiwa?

Aina zote mbili za dayalisisi ni bora kwa wagonjwa walio katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa sugu wa figo.Hakuna njia moja ambayo inaweza kusemekana kuwa inafaa zaidi kwa wagonjwa wote.Baada ya kuangalia faida na upungufu wa kila aina ya dayalisisi,uchaguzi hufanywa na mgonjwa pamoja na familia yake na daktari bingwa wa figo.Mambo muhimu ya kuangalia ni gharama ya matibabu,umri,magonjwa mengine yaliyoambatana na hali hii,umbali kutoka hospitali,kiwango cha elimu,mapendekezo ya daktari na maisha na shughuli za kawaida za mgonjwa.Kwa sababu ya gharama na kupatikana kwa urahisi,dayalisisi ya damu ndiyo hupendelewa sana na wagonjwa wengi Bara Hindi (India}.

Je,wagonjwa wanaofanyiwa dayalisisi huhitaji kuzingatia ushauri wa vyakula vyao?

Ndio,ushauri wa vyakula kwa wagonjwa wa dayalisisi huwa ni kudhibiti chumvi, potasiamu,fosforasi na vinywaji. Lazima wagonjwa wazingatie ushauri wa daktari kuhusiana na vitu hivi lakini masharti hupunguzwa baada ya dayalisisi kuanzishwa kwa wenye ugonjwa sugu wa figo.Wengi hushauriwa wale vyakula vyenye protini nyingi na vyenye kuleta nguvu nyingi,vitamini na madini.

Je, ‘Uzito mkavu’ ni upi/ nini?

Maneno ‘uzito mkavu’ hutumika sana kwa wagonjwa wa dayalisisi.Hunamaanisha uzito wa mtu baada ya umajimaji wote usiohitajika umetolewa kwa dayalisisi.‘Uzito mkavu’ unafaa kurekebishwa mara kwa mara kulingana na uzito halisi wa mgonjwa.

Hii ndiyo dayalisisi inayopendwa na kutumika sana.Kwa njia hii damu husafishwa kwa mashine na maji ya dayalisisi.

Hata baada ya dayalisisi kuanzishwa, ushauri wa vyakula uendelee na lazima uzingatiwa.

Dayalisisi ya Damu

Dayalisisi ya Damu hufanywaje?

Sana sana dayalisisi ya damu hufanyika katika vituo vya dayalisisi chini ya uangalizi wa daktari,wauguzi na mafundi wa mitambo ya dayalisisi.

  • Mashine ya dayalisisi husukuma kama mililita mia tatu ya damu kwa dakika kutoka mwilini hadi kwenye sehemu ya mashine ya kusafisha kupitia tyubu au kifuko chepesi.Dawa ya heparin huendelea kuwekwa ili damu isigande.
  • Sehemu ya mashine ya kusafisha ni kama figo bandia ambayo huchuja maji yasiyohitajika mwilini pamoja na uchafu.Husafisha damu kwa kutumia maji maalumu yanayotayarishwa kwa mashine hiyohiyo ya dayalisisi.
  • Punde damu inaposafishwa tu, mashine huirudisha mwilini.
  • Dayalisisi ya damu hufanywa kwa kawaida mara tatu kwa wiki na huchukua muda wa kama saa nne.

Damu hutolewa na kurudishwa vipi?

Njia tatu za kufikia damu kwa mishipa ni kupitia kwenye katheta iliyounganishwa na mshipa mmoja mkubwa; pili, mshipa mkubwa na mdogo kuunganishwa moja kwa moja na tatu kipandikizi cha plastiki kutumiwa kuunganisha mishipa hii.

Hemodialisis ni usafishaji wa damu unaopendwa sana kwa kutibu figo iliyo katika hatua ya mwisho ya ugonjwa.

Njia ya katheta kuunganishwa

1. Njia ya katheta kuunganishwa na mshipa mmoja mkubwa

  • Ili kuanza dayalisisi mara moja,njia ya kuingiza katheta au kifuko kwenye mshipa wa damu ndiyo njia bora na hutumiwa kwa wingi.
  • Njia hii ni nzuri ya kutumiwa kwa muda mfupi-kabla njia ya mshipa mdogo kuunganishwa kwenye mshipa mkubwa moja kwa moja au ile njia ya mishipa kuunganisha na tyubu ya plastiki kutengenezwa.
  • Katheta huingizwa kwenye mshipa mkubwa shingoni,kifuani au mguuni karibu na kinena. Kwa kutumia katheta hii zaidi ya 300ml za damu kwa dakika huweza kutolewa ili isafishwe.
  • Katheta huwa ni kifuko au tyubu iliyo na midomo miwili.Damu huingilia mdomo mmoja na kuingia kwenye mashine ya dayalisisi,kisha hurudishwa mwilini kupitia mdomo wa pili.
  • Katheta zinazounganishwa na mishipa haziwezi kutumiwa kwa muda mrefu kwa sababu ya hatari ya kuchafuka na damu kuganda.
  • Kuna aina mbili za katheta:zile zenye upenyo ambazo zinaweza kutumika kwa miezi kadha na zisizo na upenyo ambazo hutumika kwa wiki kadha tu.

Nasuri ya ateri na vana

2. Njia ya mshipa mkubwa(ateri)kuunganishwa kwa mshipa mdogo(vena)-Nasuri ya AV

  • Njia ya Nasuri ya AV ndiyo mara nyingi hutumika kwa dayalisisi ya muda mrefu kwani hudumu na ni vigumu kupata uchafu au damu kuganda.
  • Kwa njia hii ateri na vena hupasuliwa na kuunganishwa.kwa kawaida njia hii hutengenezwa kwenye mkono karibu na kifundo cha mkono.
  • Damu nyingi hutoka mshipa mkubwa wa ateri na kuingia kwenye mshipa mdogo wa vena,kwa nguvu nyingi.Baada ya wiki kadhaa au miezi,mshipa mdogo wa vena hupanuka na kubeba damu nyingi.Njia

hii ya Nasuri ya AV huchukua muda kupanuka na kuwa tayari kutumika.Haiwezi kutumiwa kufanya dayalisisi mara moja.

  • Sindano kubwa huingizwa kwenye mshipa ili kupeleka damu kwenye sehemu ya mashine ya kuisafisha na nyingine ya kurudisha damu iliyosafishwa mwilini.
  • Njia hii huweza kudumu kwa miaka mingi ikitunzwa vyema.shughuli zote za kawaida zinaweza kufanywa kwa mkono ulio na Nasuri ya AV.

Kwa nini Nasuri ya AV huhitaji utunzaji maalum?

  • Maisha ya mtu aliye katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo hutegemea dayalisisi ya mara kwa mara ili kusafisha damu.Damu ya kutosha inafaa kuweza kupitia mshipa uliotengenezwa, ili isafishwe.kwa hivyo,njia ya Nasuri ya AV ni tegemeo la uhai la mtu anayehitaji dayalisisi wakati wote.Kutunza Nusuri ya AV huhakikisha kuwa damu ya kutosha inaweza kutolewa na kwa siku nyingi.

  • Damu nyingi hupitia kwenye mishipa ya AV kwa kasi / nguvu nyingi.Mishipa hii ikiumia mtu anaweza kutokwa na damu nyingi sana na kuhatarisha maisha yake.Kwa hivyo ni muhimu kulinda mishipa hii.

Njia za kutunza mishipa yenye njia ya kutolea damu( Nasuri ya AV)

Tahadhari muhimu za kuhakikisha kuwa mishipa inaweza kutoa damu ya kutosha na kwa muda mrefu.Tahadhari hizi ni kama zifuatazo.

Zuia maambukizi
Linda Nasuri ya AV

  • Hakikisha kuwa mkono ulio na Nasuri ni safi wakati wote na kabla ya kila dayalisisi.
  • Tumia Nasuri ya AV kwa dayalisisi pekee.Usikubali yeyote atumie njia hii kudunga sindano,kutoa damu wala kupima shinikizo la damu kutumia mkono huu.
  • Chunga mishipa iliyo na Nasuri .Usivae bangili,nguo iliyobana mkono wala saa kwenye mkono huu.Mkono huu ukijeruhiwa , hata kwa bahati mbaya,damu nyingi itatoka na kuhatarisha maisha. Kudhibiti kutokwa na damu,bana mahali panapotoka damu kwa nguvu ukitumia mkono mwingine au bendeji.Damu ikikoma kutoka,Ongea na/mfahamishe daktari wako mara moja.Usijaribu kukimbia hospitalini damu inapotoka kwani hii ni hatari.Jaribu mara moja kuzuia kupoteza damu nyingi zaidi kwa kufunika na kubana panapotoka damu.
  • Usiinue kitu kizito kwa mkono ulio na Nasuri ya AV wala usiufinye Tahadhari usiulalie mkono huu.
Nasuri ya AV ndilo tegemeo la uhai la wagonjwa wa figo.Bila njia hii dayalisisi ya damu haiwezi kufanywa kwa muda mrefu.

Hakikisha kwamb a mishipa ya Nasuri ya AV inafanya kazi

  • Pima mtiririko wa damu katika Nasuri ya AV kwa kusikiliza mtetemo wa damu mara tatu kwa siku (kabla ya kiamshakinywa, chakula cha mchana na chakula cha j ioni).Iwapo mtetemo hausikiki,mfahamishe daktari wako au kituo cha dayalisisi mara moja.Kujua mapema kama Nasuri ya AV imeziba na kuitoa damu iliyoganda kunaweza kuiokoa Nasuri ya AV.
  • Shinikizo la damu lililo chini linaweza kukwamisha mishipa ya Nasuri ya AV kupeleka damu kwa hivyo ni muhimu lizuiwe.

Mazoezi
Mazoezi ya mara kwa mara yanaweza kusaidia njia ya Nasuri ya AV kukomaa haraka.Hata baada ya kuanza dayalisisi ni muhimu kuendelea kufanya mazoezi ili kuimarisha mishipa hii.

3. Njia ya Kipandikizi au kiunganishi

  • Kiunganishi kati ya mshipa mkubwa wa ateri na mdogo wa vena ni njia nyingine inayoweza kutumiwa iwapo mishipa midogo haitoshi kwa Nasuri ya AV au njia ya Nasuri ya AV imeshindwa kufanya kazi.
  • Katika njia hii,mshipa wa ateri huunganishwa na mshipa wa vena kwa kutumia kifuko au tyubu fupi nyororo inayowekwa chini ya ngozi.Sindano huingizwa kwa kipandikizi hiki wakati wa matibabu ya dayalisisi.
  • kilinganishwa na ile ya Nasuri ya AV ambapo mshipa mkubwa wa ateri huunganishwa moja kwa moja na mshipi mdogo wa vena,njia ya kipandikizi ina hatari zaidi ya damu kuganda,kupata maambukizi au kuchafuka,na haidumu kama njia ya Nasuri ya AV.
Ni muhimu kutunza mishipa ya Nasuri ya AV ili kuhakikisha inatoa damu ya kutosha na pia inatumika kwa muda mrefu.

Kazi za mashine ya dayalisisi ni zipi?

Kazi muhimu za mashine ya dayalisisi ni kama zifuatazo:

  • Mashine hii husukuma damu na kufuatia mtiririko wa damu kutoka mwilini hadi kwenye mashine inaposafishwa damu.
  • Mashine hutengeneza maji maalumuya kusafisha damu.Mashine hufuatia na kusawazisha joto,kiasi na kasi ya maji ya dayalisisi ambayo yanafaa kulinganishwa na mahitaji ya mgonjwa kwa uangalifu mkubwa. Maji haya hutoa uchafu na maji yasiyohitajika mwilini.
  • Kwa usalama wa mgonjwa,mashine ya dayalisisi ina vifaa tofauti vinavyoweza kugundua uvujaji wa damu kutoka kwenye mashine au kuwepo kwa hewa katika mzunguko wa damu.
  • Kwa mashine zilizo na kompyuta, mashine hizi huonyesha vipimo mbalimbali na huonya iwapo kuna kasoro huhakikisha hakuna matatizo,kuna usahihi, usalama na kufuatiliwa wakati wote dayalisisi inapofanywa.

Muundo wa sehemu ya mashine inayosafisha damu na jinsi inavyofanya kazi?

  • Katika dayalisisi sehemu hii ni kichungi(figo bandia)ambacho husafisha damu.
  • Kichungi hiki huwa na urefu wa sentimita kama ishirini hivi na upana wa kama sentimita tano.Ni silinda ya plastiki yenye maelfu ya nyuzi kama tyubu zenye utando unaoweza kupenyeka.
Mashine ya dalisisi, ikisaidiana na maji ya dialiaza, huchuja damu na hudumisha ugiligili,kiasi cha madini na asidi mwilini.
  • Nyuzi hizi huungana upande wa juu na wa nchini wa silinda na kutengeneza ‘chumba cha damu’.Damu huingia chumba hiki kwa mdomo mmoja na kutoka kwa mdomo wa pili baada ya kusafishwa.
  • Maji ya dayalisisi huingi lia mdomo mmoja,huzunguka nje ya nyuzi na kutengeneza chumba cha maji na kutokea kwa mdomo mwingine.
Usafishaji wa damu katika mashine
  • Katika dayalisisi,damu inayosukumwa na mashine huingia kwa mdomo mmoja na husambazwa kwenye nyuzi zinazofanana na mishipa midogomidogo kabisa ya damu.
  • Kwa kila dakika,karibu mililita mia tatu ya damu na mililita mia sita ya maji ya dayalisisi hutiririka kutoka pande zote mbili za mashine.Utando wa nyuzi unaotenga damu na maji hupenyeka ( semi-permeable)na hivyo kuwezesha uchafu na maji yasiyohitajika kutoka na kuingia kwenye‘chumba cha maji’.
  • Damu hutokea mwisho huo mwingine wa mashine baada ya kusafishwa.Maji yenye uchafu uliotolewa kwenye damu nayo hutokea kwenye upande wa mashine ambao damu huingilia.
  • Kwa njia hii damu yote ya mwili husafishwa mara kumi na mbili hivi.Mwishoni mwa kazi hii ya saa nne,yurea ya damu,maji yasiyohitajika, kreatinini na chumvichunvi (electrolytes) hupungua sana.

Je,maji ya dayalisisi ni nini na kazi yake ni ipi?
  • Maji haya ni maalum na hutumika kutoa uchafu na umajimaji usiohitajika kwenye damu.
  • Maji haya kwa kawaida hufanana na maji ya kawaida yaliyoko mwilini lakini huweza kubadilishwa kulingana na mahitaji ya mgonjwa.
  • Maji hutengenezwa na mashine ya dayalisisi kwa kuchanganya sehemu thelathini za maji yaliyosafishwa kwa hali ya juu na sehemu moja ya dawa ya dayalisisi(30.1).
  • Dawa hii ni maji maalum yanayouzwa kwenye chupa na huwa yamekolea chumvichumvi (electrolytes), madini na bikabonati.
  • Ili kutayarisha maji ya dayalisisi,maji ya kawaida yanayoingia kwenye mashine husafishwa kwa njia kadha kwa kutumia kichungi cha changarawe na cha makaa,kutoa chumvi chumvi na njia zingine za kisayansi kama vile reverse osmosis, deionization, na kuchuja kwa miale ya ultra violet.(ultra violet filtration).
  • Maji yaliyosafishwa kiasi hiki huwa hayana vumbi,uchafu mwingine unaoelea,uchafu wa kikemikali,madini, bacteria au sumu za ndani (endo-toxins).

  • Maji yaliyosafishwa kwa hali ya juu ni muhimu kwa usalama wa dayalisisi kwani karibu lita mia moja na hamsini hutumiwa kwa kila dayalisisi.
  • Ili kumkinga mgonjwa na hatari ya uchafu wa maji,lazima maji yasafishwe kwa umakini mkubwa na pia yaendelee kuangaliwa yanapotumiwa.

Dayalisisi ya damu hufanywa wapi?

Kwa kawaida,dayalisisi ya damu hufanywa hospitalini au kwenye kituo cha dayalisisi chini ya wahudumu waliohitimu wakiongozwa na daktari.Kwa wagonjwa wachache,dayalisisi huweza kufanywa nyumbani.Hii huwezekana tu kwa wagonjwa ambao hali yao imeimarika na huhitaji mafunzo mazuri,usaidizi wa familia, nafasi ya kutosha na fedha za kutosha.

Je, dayalisisi ina uchungu/maumivu? Mgonjwa hufanya nini wakati wa dayalisisi?

Hapana.Dayalisisi haina uchungu isipokuwa wakati sindano inapoingizwa.Mgonjwa anayefanyiwa dayalisisi ya kawaida huenda hospitalini na kurudi nyumbani baada ya dayalisisi.

Kwa kawaida wagonjwa hupumzika au hulala wakati wa saa nne za dayalisisi.Wanaweza pia kusoma,kusikiliza muziki, au hata kutazama runinga.Wakati wa dayalisisi wagonjwa hupendelea kupewa viburindisho vyepesi au vinywaji baridi.

Dayalisisi ina matatizo yapi?

Matatizo ya kawaida wakati wa dayalisisi huwa kama shinikizo la damu kwenda chini (hypotension),kichefuchefu au kutapika,mkakamao wa misuli (cramps), uchovu na kuumwa na kichwa.

Maji ya dialisi hurekebisha na kuleta usawa wa madini mwilini kwa kuondoa uchafu wakati wa kusafisha damu kwa hemo dialisisi.

Faida na kasoro za dayalisisi ya damu:
Faida za dayalisisi ya damu

  • Hufanywa na wauguzi waliohitimu au mafundi wa dayalisisi,kwa hiyo huwa salama na isiyo na usumbufu kwa wagonjwa.
  • Dayalisisi ya damu ni haraka na yenye utendaji bora kwa hiyo huchukua muda mfupi kuliko dayalisisi ya tumbo.
  • Dayalisisi ya damu huwezesha wagonjwa kukutana na wengine walio na shida kama zao.Utangamano huu hupunguza mfadhaiko na mgonjwa anaweza kufurahia uwepo wa wagonjwa wenzake.
  • Humpa mgonjwa uhuru zaidi kwani hufanywa kwa siku tatu tu kwa wiki.
  • Hatari ya maambukizo ni kidogo.
  • Dayalisisi ya damu ni rahisi ukilnganisha na ya tumbo katika vituo vingi.

Matatizo Ya Dayalisisi Ya Damu

  • Usumbufu wa mgonjwa kwenda mara kwa mara kwenye kituo cha dayalisisi na hasa kama kituo hicho kipo mbali.
  • Mgonjwa lazima apange ili atimize mahitaji / matakwa ya mpango mzima wa dayalisisi.
  • Udungwaji wa sindano una maumivu.
  • Mgonjwa hana uhuru wa vyakula- Mgonjwa aliye kwenye dayalisisi ya damu lazima afuate maelekezo ya maji (fluids), chumvi,potasiam, na pia vyakula vilivyo na fosfarasi nyingi.
  • Wagonjwa wanaofanyiwa dayalisisi ya damu wana hatari zaidi ya kupata /kuambukizwa homa ya maini.
Faida kuu za dayalisisi ya damu ni usalama,ubora na haina usumbufu.

Vitu Gani Wagonjwa Wa Dayalisisi Wafanye Na Vipi Wasifanye

  • Wagonjwa walio na ugonjwa sugu wa figo (ESKD)na ambao wanatibiwa kwa dayalisisi, wanahitaji kwenda kufanyiwa dayalisisi mara tatu kwa juma bila kukosa. Kwenda kufanyiwa dayalisisi ni muhimu kwa afya njema kwa muda mrefu, kutokufuata maelekezo ya kufanyiwa dayalisisi ni hatari na kunaweza kusababisha hata kifo.
  • Kutokunywa maji mengi (fluids) na kula chumvi ni muhimu ili kuzuia ongezeko la uzito hasa katikati ya miula ya dayalisisi. Mgonjwa asile vyakula vilivyo na potasiam na fosforasi nyingi. Ale protini zaidi.
  • Utapiamlo hutokea mara nyingi kwa wagonjwa walio kwenye dayalisisi na ikitokea hivyo maendeleo yao hayawi mazuri : wanaweza hata kupoteza maisha. Kutokula protini yakutosha na upotevu wa protini wakati wa dayalisisi, upelekea mgonjwa kuwa na utapiamlo. Kwa hiyo mgonjwa aliye kwenye dayalisisi ale chakula chenye protini na chakula kinacholeta nguvu barabara.
  • Wagonjwa wa dayalisisi wanafaa kupewa vitamini zinazoweza kuyeyuka kwenye maji kama vile B na C. Wasishauriwe kununua dawa za vitamini madukani kwani zinaweza kuwa hazina ubora, hazina vitamini zote zinazohitajika au iwe vitamini zilizomo si za kutosha kwa mgonjwa wa dayalisisi,au pengine ziwe na vitamini zenye madhara kama vile A, E na K au madini.
  • Madini ya kalsiamu (iliyo kwenye mifupa na meno) na vitamini ya D vinaweza kupatiwa mgonjwa kutegemea viwango vya madini alivyo navyo (ikiwa pamoja na kiasi cha kalsiam,fosfarasi, na kiwango cha parathairoid homoni).
  • Lazima mgonjwa azingatie ushauri kama kuzuia kunywa pombe,kutovuta sigara,kudumisha uzito unaofaa,kufanya mazoezi na kadhalika.
Kizuizi/ugumu mkubwa wa hemodialisisi ni mgonjwa kuhitajika kwenda hospitali mara tatu kila juma.

Dayalisisi Ya Tumbo

Ni wakati gani mgonjwa inafaa amwone muuguzi au daktari?
Mgonjwa aliye kwenye dayalisisi inafaa amwone muuguzi wa dayalisisi au daktari wake mara moja iwapo:

  • Anatokwa na damu kwenye mkononi wenye Nasuri ya AV au mahali katheta imewekwa.
  • Mtetemo wa mtiririko wa damu hausikiki kwenye mkono ulio na Nasuri ya AV.
  • Uzito ukiongezeka ghafla,kuvimba au akiwa na shida ya kupumua.
  • Maumivu ya kifua na mdundo wa moyo usio wa kawaida.
  • Shinikizo la damu kuwa juu zaidi au chini zaidi.
  • Mgonjwa kuchanganyikiwa,kuzimia au kusinzia.
  • Mgonjwa anahisi baridi sana na kutetemeka,kutapika sana au kutapika damu au/na kukosa nguvu kwa ujumla.

Dayalisisi Ya Tumbo

Dayalisisi ya tumbo,hii ni njia nyingine ya dayalisisi kwa wagonjwa walio katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo (ESKD).Hutumika sana nyumbani.

Kwa wagonjwa wa hemodialisisi uzuiaji wa maji na chimvi ni muhimu ili uzito usiongezeke hasa kati ya dialisisi.

Dayalisisi ya wakati wote

Dayalisisi ya tumbo ni nini?

  • Dayalisisi hii hufanywa kupitia utando(membrane) unaozunguka tumbo,matumbo na sehemu zingine za tumbo.
  • Utando huu wa tumbo una ruhusu kupenyeza uchafu na sumu ulio kwenye damu kupitia kwake na kuutoa.
  • Dayalisisi ya tumbo ni njia ya kusafisha damu kupitia kwenye utando huu.

Aina za dayalisisi ya tumbo

    1. Dayalisisi ya vipindi vifupi vifupi.(IPD)
    2. Dayalisisi ya wakati wote.(CAPD)
    3. Dayalisisi inayojiendesha.(CCPD)

1. Dayalisisi ya vipindi vifupi vifupi (Intermittent Peritoneal Dialysis - IPD)

Aina hii ya dayalisisi ya tumbo ni bora kwa wagonjwa walio hospitalini wanaohitaji dayalisisi kwa muda mfupi tu.Hutumika sana kwa watu wenye ugonjwa wa figo wa muda,kwa watoto na katika hali ya dharura kwa wagonjwa walio katika kipindi cha mwisho cha ugonjwa wa figo.

  • Katika njia hii,katheta ya plastiki yenye vishimo vingi huwekwa kwenye tumbo pamoja na maji maalum ya dayalisisi.
  • Dayalisisi hii hufanywa kwa muda wa saa 24 hadi saa 36 na takriban lita thelathini au arobaini za maji maalum ya dayalisisi hutumika kwa kila kipindi cha matibabu.
  • Dayalisisi aina hii hurudiwa baada ya kati ya siku moja hadi tatu kulingana na mahitaji ya mgonjwa .
CAPD ni aina ya dialisisi inayoweza kufanywa na mgonjwa mwenyewe nyumbani akitumia maji maalumu (special fluid).

CAPD

2. Dayal isisi ya wakati wote.(Continous Ambulatory Peritoneal Dialysis - CAPD)

  • Dayalisisi hii hufanywa kwa mfululizo,saa ishirini na nne za siku na siku saba za wiki.
  • Mgonjwa anaweza kutembea na kufanya shughuli za kawaida.
  • Utando wa tumbo ndio hutumika kama kichungi.

Njia hii inaweza kutumiwa na mgonjwa nyumbani bila ya kutumia mashine.kwa sababu njia hii inampa mgonjwa uhuru wa kuendelea na shughuli zake. Hutumiwa sana katika nchi zilizoendelea.

Hufanywaje?

Njia hii ya dayalisisi hutumia katheta nyepesi na laini yenye vishimo vingi . Katheta hii huingizwa kwa njia ya upasuaji kwenye tumbo la mgonjwa. Katheta hii ni njia ya kudumu ya dayalisisi.Huingizwa kwenye tumbo kama inchi moja (1") chini na kwa upande wa kitovu.Katheta huwekwa siku kumi hadi kumi na nne kabla ya dayalisisi kuanza.kama vile Nasuri ya AV, katheta hii ndiyo ‘tegemeo la uhai’ la mgonjwa.

Hatua za dayalisisi ya wakati wote

Njia hii ya dialisisi ina hatua tatu: kujaza,kukaa na kutoa maji.
Kujaza: kupitia katheta,lita mbili za maji ya dayalisisi ya tumbo yaliyowekwa kwenye mfuko safi kabisa hutiririshwa tumboni.Maji haya yakishawekwa tumboni huwa yanagusana na utando wa tumboni (peritoneum). Mfuko wake mtupu hukunjwa na kuwekwa kwenye nguo ya ndani ya mgonjwa hadi wakati mwingine wa matibabu.
Kukaa: Maji ya dayalisisi hukaa tumboni kwa saa nne hadi sita wakati wa mchana na saa sita hadi nane wakati wa usiku. Wakati ambapo maji yaliyowekwa kwenye hatua ya kujaza na yapo tumboni, huitwa wakati waKUKAA. Huu ndio wakati damu inasafishwa .Utando wa tumbo ndio huwa kama kichungi kinachoruhusu uchafu kupita kutoka kwenye damu na kuingia kwenye maji . Wakati haya yanapoendelea,mgonjwa yuko huru kutembea.

CAPD iendeshwe kwa uangalifu na usafi mkubwa kila siku kwa wakati uleule hata wakati wa sikukuu.

Dayalisisi inayojiendesha

Kutoa maji: Baada ya kukaa,maji ya dayalisisi yaliyo na uchafu hutolewa kupitia katheta na kuingia kwenye mfuko uliowekwa kwenye nguo ya ndani ya mgonjwa. Mfuko uliokusanya maji hupimwa uzito na baadae kutupwa Maji yaliyokusanywa yanapaswa yasiwe na rangi yoyote.

Kutoa maji tumboni na kujaza maji mapya huitwa kubadilisha. Kunawezwa kufanywa mara tatu hadi tano wakati wa mchana na mara moja wakati wa usiku.Wakati wa usiku,kubadilisha hufanywa kabla ya mgonjwa hajalala na maji huachwa tumboni usiku kucha.Shughuli hii lazima ifanywe kwa mazingira na njia ya usafi kabisa.

3. Dayalisisi inayojiendesha.

Hii ni dayalisisi inayoendelea wakati wote kwa kutumia mashine.Hufanyw anyumbani.Mashine

Dialisisi inayojiendesha hujaza na kutoa maji ya dayalisisi tumboni.kila mzunguko wa kujaza na kutoa huchukua kama saa moja hadi mbili na kubadilisha hufanyika mara nne au tano.kazi hii yote huchukua muda wa kama saa nane hadi kumi mgonjwa alalapo usiku.Mashine inapotolewa asubuhi,lita mbili hadi tatu za maji ya dayalisisi huachwa tumboni.Maji haya hubaki tumboni hadi jioni yanapotolewa na mashine kuwekwa tena.

Faida kuu za njia hii ni kuwa na uhuru wa kufanya shughuli za kawaida za mchana na kwamba mashine huwekwa mara moja na kutolewa mara moja tu kwa siku.Hii humwezesha mgonjwa kupumzika na hupunguza hatari ya utando wa tumbo kupata maambukizi yanayosababisha kuvimba.(peritonitis). Lakini ikumbukwe njia hii ni ghali.

Dialisisi ya peritoni hufanyika nyumbani kwa kutumia mashine maalumu inayojiendesha, (automated cycler machine).

Maji yanayotumika katika dayalisisi ya kudumu au wakati wote ni yapi?

Maji yanayotumika huwa ni maji safi kabisa yenye madini na sukari( glukosi) yanayotumika katika dayalisisi.Kutegemea kiwango cha Sukari,maji haya huwa yana nguvu tofauti.kuna yenye kiwango cha asilimia 1.5% ,2.5 % na 4.5%. Glukosi iliyo kwenye maji haya ndiyo huwezesha maji kutolewa mwilini.Maji yenye nguvu tofauti hutumiwa kulingana na kiwango cha maji yanayohitajika kutolewa mwilini.Iwapo maji mengi yanahitajika kutolewa mwilini basi maji ya dayalisisi yenye nguvu zaidi hutumiwa.

Sasa kuna aina mpya ya maji ya dayalisisi yenye nguvu zaidi yanayotumika. Maji haya huitwa icodextrin na hutumika badala ya dextrose. Faida ya maji haya mapya ni kuwa huweza kutoa maji yasiyohitajika mwilini polepole. Maji haya mapya ya dayalisisi pia ni mazuri hasa/hata kwa watu wenye kisukari au wenye uzito mkubwa. Matumizi yake huwa ni ya mzunguko mmoja tu kwa siku. Hupatikana kwenye mifuko ya mililita elfu moja hadi elfu mbili mia tano.

Matatizo ya dayalisisi ya wakati wote au ya kudumu.
1. Maambukizi

Tatizo kubwa sana kwa mgonjwa anayefanyiwa dayalisisi hii huwa ni ugonjwa wa uvimbe wa utando uliozunguka sehemu za ndani za tumbo(fumbatio),maumivu ya tumbo,dalili za homa,kibaridi na maji ya dayalisisi kuonekana machafu yanapotoka mwilini zote huwa ni dalili za ugonjwa huu wa uvimbe wa fumbatio. Ili kuzuia ugonjwa huu,lazima dayalisisi ifanywe kwenye mazingira safi kabisa na kuhakikisha kuwa mgonjwa hafungi choo.Matibabu yake huwa ni pamoja na dawa za antibayotiki.Maji ya Dayalisisi yanayotoka mwilini yapimwe ili kujua dawa sahihi zitakazofaa kutumiwa na kwa wagonjwa wengine katheta hutolewa, kwani mahali katheta ilipoingizwa panaweza kuwa ndiyo chanzo cha maambukizi.

Matatizo mengine

Kuvimba tumbo,kudhoofika kwa misuli ya tumbo na kusababisha ngiri,maji kuzidi mwilini,mfuko wa korodani kuvimba/kujaa maji,kufunga choo,kuumwa na mgogo,maji kutotoka vizuri,maji ya dayalisisi kuvuja na mgonjwa kuongeza uzito.

Faida za dayalisisi ya wakati wote
  • Masharti ya vyakula na vinywaji huwa si makali sana. Uangalifu mkubwa unahitajika ili kuzuia maambukizi kuwapata wagonjwa wanaofanyiwa dayalisisi ya kudumu.

  • Mgonjwa huwa huru zaidi kwani dayalisisi inaweza kufanyika nyumbani,kazini na hata anaposafiri. Shughuli za kawaida huweza kuendelea wakati dayalisisi inapofanyika.Mgonjwa anaweza kujifanyia dayalisisi kwani hahitaji mashine, wala daktari,wala jamaa.
  • Mgonjwa hana haja ya kwenda hospitalini mara tatu kama kawaida,wala kusafiri wala kudungwa sindano.
  • Shinikizo la damu na anemia huzuilika kwa njia bora zaidi.
  • Njia hii huwezesha damu kuendelea kusafishwa wakati wote kwa hivyo hakuna usumbufu.

Mapungufu wa dayalisisi ya kudumu

  • Hatari ya maambukizi kwenye utando wa tumboni au panapopitia katheta.
  • Mgonjwa anatakiwa kubadilisha mara tatu hadi tano kila siku ya maisha yake(exchange) Kuzingatia maagizo na usafi wa hali ya juu kila wakati, hii si kazi rahisi.
  • Kuwa na katheta na maji tumboni kila wakati haina raha na pia,wengi huwa hawapendi jinsi mwili unavyoonekana.
  • Sukari iliyo katika maji ya dayalisisi inaweza kumfanya mgonjwa aongeze uzito au kuwa na sukari zaidi mwilini.
  • Kuiweka mifuko mizito ya dayalisisi nyumbani si rahisi.
Faida kubwa ya CAPD ni uhuru wa mahali na wakati na pia makatazo ya vyakula ni kidogo.

Mashauri ya mlo

Ushauri wa vyakula kwa mgonjwa anayefanyiwa dayalisisi kwa mashine inayojiendesha huwa muhimu sana.pia, huwa tofauti na ule wa anayefanyiwa dayalisisi ya damu kupitia kwenye mishipa.

  • Vyakula vyenye protini nyingi ni muhimu ili kuzuia ukosefu wa protini mwilini kwa sababu ya kupoteza protini nyingi katika dayalisisi ya tumbo.
  • Zuia vyakula vyenye joto jingi ili kuzuia kuongeza uzito ,maji ya dayalisisi huwa na sukari ya glukosi ambayo huzidi kuongeza kabohaidriti kwa mwili wa mgonjwa.
  • Masharti ya matumizi ya chumvi na vinywaji ni mepesi hapa kuliko kwa wagonjwa wanaofanyiwa dayalisisi kwenye mishipa ya damu.
  • Kuzuia vyakula vyenye potasiamu na fosfati.
  • Ale zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi ili kuzuia kufunga choo.

Ni wakati gani mgonjwa aende kwa daktari au muuguzi wake wa dayalisisi?

  • Akipata maumivu ya tumbo,dalili za homa au kutetemeka.
  • Iwapo maji ya dayalisisi yanayotoka mwilini yanaonekana machafu au yana damudamu.
  • Uchungu,usaha,wekundu,kuvimba au joto mahali ambapo katheta inatokea.
  • Mtiririko wa maji (fluid) ndani au nje ya tumbo umeziba au mgonjwa hapati choo (constipation).
  • Kuongeza uzito ghafla, kuvimba mwili,kushindwa kupumua au shinikizo la damu kuwa juu sana (inahashiria kuongezeka ghafla kwa maji mwilini).
  • Shinikizo la damu la chini,kupungua uzito, mkakamao wa misuli (cramps) au kizunguzungu. (kunahashiria upungufu wa maji –fluid).
Wagonjwa wa dayalisisi ya wakati wote sharti wale vyakula vyenye protini nyingi ili kuzuia maambukizi na utapiamlo.